Friday, 7 March 2014

MJUE SHUJAA ALIYEITANGAZA TANZANIA KITAIFA NA KIMATAIFA KUPITIA MADINI ALIYOYAVUMBUA.




Mvumbuzi, Mzee Jumanne Mhero Ngoma





KILA mwaka, madini aina ya Tanzanite huiingizia Tanzania kiasi cha dola milioni 20 (zaidi ya Sh bilioni 30). Duniani kote, madini hayo hayo huingiza wastani wa dola milioni  500 (zaidi ya Sh bilioni 800).
Wakati mabilioni yote hayo yakiingia mfukoni mwa serikali na wafanyabiashara, mgunduzi wa madini hayo, Jumanne Mhero Ngoma (74), anaishi kwa kutegemea ruzuku za watoto. Mapato yake kwa mwaka ni shilingi za Tanzania sifuri!
 Nilikutana na Mzee Ngoma siku chache zilizopita jijini Dar es Salaam katika ofisi ya mmoja wa wanawe. Pamoja na masahibu na mikasa mbalimbali iliyomkumba katika maisha yake, bado aliweza kunipokea kwa bashasha na tabasamu.
 Amefanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari na pengine ameanza kuchoka sasa. Mvi kichwani kwake na kwenye eneo la ndevu ni ishara kwamba umri unaanza kumtupa Mzee Ngoma.
Nimekaa namtazama. Huyu ndiye mtu aliyegundua madini ya Tanzanite. Alipaswa kuwa utambulisho wa Watanzania. Katika nchi nyingine zinazothamini watu wake, huyu alitakiwa kufahamika na watu wote waliomaliza elimu ya msingi.
 Kama ambavyo watoto wote wa Kimarekani wanavyomfahamu Thomas Edison (mbunifu mashuhuri na mfanyabiashara wa karne kadhaa zilizopita) . Lakini mbele ya macho yangu, alikaa mzee mmoja ambaye kama ningekutana naye kwenye daladala (na ndiyo usafiri wake mkuu), nisingemtazama mara mbili.
 Namuuliza swali moja la msingi kwamba ilikuwaje yeye aliyagundua madini ambayo wakoloni (wazungu) walishindwa kuyabaini kwa muda wote waliokaa hapa nchini.
“Nakumbuka kila kitu kuhusu mara yangu ya kwanza kuona madini hayo. Mara ya kwanza kuyagundua madini haya nilikuwa mdogo sana. Nilikuwa na umri wa chini ya miaka 20 na nilikuwa porini nikichunga mifugo.
 “Nilikuwa kwenye msitu ambao Wamasai walikuwa wameupa jina la Lalouo. Eneo ambako niliyaona lilikuwa linafahamika kwa jina la Naisunyai  ambako kwa kawaida Wamasai walikuwa wakilitumia kunywesha mifugo yao.
 “Siku hiyo niliona vitu vinavyowaka. Nikawa nashangaa vitakuwa ni vitu gani. Awali nilidhani pengine ni nyoka au wanyama wa hatari. Nikasogea nikiwa na upinde na mshale wangu tayari kwa lolote.
“Nilipogusa na mti niliokuwa nimeushika, nikashangaa mawe yanayong’aa yakitoka ardhini. Vipande vidogo vidogo vyenye rangi ya bluu. Kwa kweli nilivipenda sana.
 “Nilishangaa sana lakini ghafla nikakumbuka kuwa nilikuwa nachunga mifugo. Kumbe ng’ombe na mbuzi niliokuwa nawachunga walikuwa wamekimbia tayari. Nikaacha shughuli hiyo na kwenda kuwafuata.

.........................................itaendelea kesho......................................
source: RAIA MWEMA NEWSPAPER

No comments: