Wednesday, 21 May 2014

WADAU WA UONGEZAJI THAMANI MADINI WAFANYA MKUTANO JIJINI DAR

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Celestine Onditi wa pili kulia amabaye alikua mgeni rasmi katika mkutano wa wadau wa ukusanyaji maoni sheria ya uongezekaji thamani madini akiwa katika picha ya pamoja na wadau hao. Wakwanza kushoto ni kamishna msaidizi wa sheria ya uongezaji thamani madini, mhandisi  Hamisi Komba,(wa tatu kushoto) ni kamishna msaidizi wa uchumi na biashara mhandisi Salim  Salim, kamishna msaidizi wa madini kanda ya kusini mhandisi Benjamin Mchwampaka wa kwanza kulia ni kamishna msaidizi wa kanda magharibi Shubi Byabota.


Mhandisi madini na uchenjuaji migodi Wizara ya Nishati na Madini, Bi. Asnath Mkani akiwasilisha mada ya historia ya uongezaji thamani madini nchini.

Baadhi ya wadau wa sheria ya uongezaji thamani madini wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa mkutano huo.

Katibu tawala wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Celestine Onditi akisalimiana na baadhi ya wadau wa sheria ya uongezaji thamani madini mara baada ya kufungua mkutano huo.

                    Na Hamisi Yassn, Dar es salaam

Katika picha ni mkutano wa wadau wa sheria ya uongezaji thamani madini unaoendelea jijini dar es salaam baada ya mkutano kama huo uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha. Mikutano hiyo inafanyika ili kupata maoni ya wadau wa tasnia ya madini ya vito na usonara kwa ajili ya rasimu ya sheria hiyo.


Wakati akifungua mkutano huo jana, katibu tawala wa Wilaya ya Kinondoni  Bw. Celestine Onditi aliwataka wadu kutoa maoni yao ili iweze kupatikana sheria ambayo itakuwa ni shirikishi akiunganisha maoni ya wadau wote wa sekta ya madini hali itakayo saidia. Ameongeza endapo wadau watatoa maoni  stahiki sheria hiyo itasaidia sekta ya madini kuchangia kwa pato la Serikali kwa kiasi kikubwa zaidi ikizingatia kuwa nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa na hazina kubwa ya madini ya aina mbalimbali.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mgesa Mulongo wakati akifungua mkutano kama huo jijini Arusha aliwataka wadau wa sheria kutoa maoni yatakayosaidia sheria hiyo kuwa yenye tija kwa manufaa ya taifa na Watanzania.

Friday, 7 March 2014

MJUE SHUJAA ALIYEITANGAZA TANZANIA KITAIFA NA KIMATAIFA KUPITIA MADINI ALIYOYAVUMBUA.




Mvumbuzi, Mzee Jumanne Mhero Ngoma





KILA mwaka, madini aina ya Tanzanite huiingizia Tanzania kiasi cha dola milioni 20 (zaidi ya Sh bilioni 30). Duniani kote, madini hayo hayo huingiza wastani wa dola milioni  500 (zaidi ya Sh bilioni 800).
Wakati mabilioni yote hayo yakiingia mfukoni mwa serikali na wafanyabiashara, mgunduzi wa madini hayo, Jumanne Mhero Ngoma (74), anaishi kwa kutegemea ruzuku za watoto. Mapato yake kwa mwaka ni shilingi za Tanzania sifuri!
 Nilikutana na Mzee Ngoma siku chache zilizopita jijini Dar es Salaam katika ofisi ya mmoja wa wanawe. Pamoja na masahibu na mikasa mbalimbali iliyomkumba katika maisha yake, bado aliweza kunipokea kwa bashasha na tabasamu.
 Amefanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari na pengine ameanza kuchoka sasa. Mvi kichwani kwake na kwenye eneo la ndevu ni ishara kwamba umri unaanza kumtupa Mzee Ngoma.
Nimekaa namtazama. Huyu ndiye mtu aliyegundua madini ya Tanzanite. Alipaswa kuwa utambulisho wa Watanzania. Katika nchi nyingine zinazothamini watu wake, huyu alitakiwa kufahamika na watu wote waliomaliza elimu ya msingi.
 Kama ambavyo watoto wote wa Kimarekani wanavyomfahamu Thomas Edison (mbunifu mashuhuri na mfanyabiashara wa karne kadhaa zilizopita) . Lakini mbele ya macho yangu, alikaa mzee mmoja ambaye kama ningekutana naye kwenye daladala (na ndiyo usafiri wake mkuu), nisingemtazama mara mbili.
 Namuuliza swali moja la msingi kwamba ilikuwaje yeye aliyagundua madini ambayo wakoloni (wazungu) walishindwa kuyabaini kwa muda wote waliokaa hapa nchini.
“Nakumbuka kila kitu kuhusu mara yangu ya kwanza kuona madini hayo. Mara ya kwanza kuyagundua madini haya nilikuwa mdogo sana. Nilikuwa na umri wa chini ya miaka 20 na nilikuwa porini nikichunga mifugo.
 “Nilikuwa kwenye msitu ambao Wamasai walikuwa wameupa jina la Lalouo. Eneo ambako niliyaona lilikuwa linafahamika kwa jina la Naisunyai  ambako kwa kawaida Wamasai walikuwa wakilitumia kunywesha mifugo yao.
 “Siku hiyo niliona vitu vinavyowaka. Nikawa nashangaa vitakuwa ni vitu gani. Awali nilidhani pengine ni nyoka au wanyama wa hatari. Nikasogea nikiwa na upinde na mshale wangu tayari kwa lolote.
“Nilipogusa na mti niliokuwa nimeushika, nikashangaa mawe yanayong’aa yakitoka ardhini. Vipande vidogo vidogo vyenye rangi ya bluu. Kwa kweli nilivipenda sana.
 “Nilishangaa sana lakini ghafla nikakumbuka kuwa nilikuwa nachunga mifugo. Kumbe ng’ombe na mbuzi niliokuwa nawachunga walikuwa wamekimbia tayari. Nikaacha shughuli hiyo na kwenda kuwafuata.

.........................................itaendelea kesho......................................
source: RAIA MWEMA NEWSPAPER